Genesis 46

Yakobo Aenda Misri

1Hivyo Israeli akaondoka na vyote vilivyokuwa mali yake, naye alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaki baba yake.

2 aMungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!”

Akajibu, “Mimi hapa.”

3 bMungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako, usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa. 4 cNitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yosefu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.”

5 dNdipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao aliyokuwa amempelekea kumsafirisha. 6 eWakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani, Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri. 7Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote mpaka Misri.

8Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli (Yakobo na wazao wake), waliokwenda Misri:

Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.
9Wana wa Reubeni ni:
Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi.
10 fWana wa Simeoni ni:
Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani.
11Wana wa Lawi ni:
Gershoni, Kohathi na Merari.
12 gWana wa Yuda ni:
Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera (lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani).
Wana wa Peresi ni:
Hesroni na Hamuli.
13Wana wa Isakari ni:
Tola, Puva, Yashubu na Shimroni.
14 hWana wa Zabuloni ni:
Seredi, Eloni na Yaleeli.
15 iHawa ndio wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padan-Aramu pamoja na binti yake Dina. Jumla ya wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu.

16 jWana wa Gadi ni:
Sefoni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli.
17 kWana wa Asheri ni:
Imna, Ishva, Ishvi na Beria.
Dada yao alikuwa Sera.
Wana wa Beria ni:
Heberi na Malkieli.
18Hawa ndio watoto Zilpa aliomzalia Yakobo, ambao Labani alimpa binti yake Lea; jumla yao walikuwa kumi na sita.

19Wana wa Raheli mke wa Yakobo ni:
Yosefu na Benyamini.
20 lHuko Misri, Asenathi binti wa Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni,
Yaani Heliopoli (Mji wa Jua).
alimzalia Yosefu wana wawili, Manase na Efraimu.
21 nWana wa Benyamini ni:
Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi.
22Hawa ndio wana wa Raheli aliomzalia Yakobo; jumla yao ni kumi na wanne.

23Mwana wa Dani ni:
Hushimu.
24 oWana wa Naftali ni:
Yaseeli, Guni, Yeseri na Shilemu.
25 pHawa walikuwa wana wa Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alikuwa amempa Raheli binti yake; jumla yao walikuwa saba.

26 qWote waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, waliokuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe zake, walikuwa watu sitini na sita. 27 rPamoja na wana wawili waliozaliwa na Yosefu huko Misri, jumla yote ya jamaa ya Yakobo, waliokwenda Misri, walikuwa sabini.

28 sBasi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yosefu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni, 29 tgari kubwa zuri la Yosefu liliandaliwa, naye akaenda Gosheni kumlaki baba yake Israeli. Mara Yosefu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu.

30 uIsraeli akamwambia Yosefu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.”

31 vNdipo Yosefu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu. 32 wWatu hao ni wachunga mifugo, huchunga mifugo, wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ngʼombe pamoja na kila kitu walicho nacho.’ 33 xFarao atakapowaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’ 34 yMjibuni, ‘Watumwa wako wamekuwa wachunga mifugo tangu ujana wetu mpaka sasa, kama baba zetu walivyofanya.’ Ndipo mtakaporuhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wachunga mifugo wote ni chukizo kwa Wamisri.”

Copyright information for SwhNEN